Local News

Rais Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Idara ya Upasuaji wa Ubongo na Mishipa kutoka Hospitali ya Kimataifa ya Chuo Kikuu cha Peking (PUIH) iliyopo Beijing nchini China.

Rais Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Idara ya Upasuaji wa Ubongo na Mishipa kutoka Hospitali ya Kimataifa ya Chuo Kikuu cha Peking (PUIH) iliyopo Beijing nchini China.

Clement Silla

February 26th, 2019

No comments

Rais Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Idara ya Upasuaji wa Ubongo na Mishipa kutoka Hospitali ya Kimataifa ya Chuo Kikuu cha Peking (PUIH) iliyopo Beijing nchini China Prof. Zhao Yuanil ambaye ameongoza timu ya wataalamu wanaoshirikiana na Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili MOI katika Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu.

Mazungumzo hayo yamefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Balozi wa China hapa nchini Wang Ke, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Mseru.

Katika mazungumzo hayo Rais Magufuli ameishukuru Hospitali ya Kimataifa ya Chuo Kikuu cha Peking kwa kukubali ombi lake la kuanzisha ushirikiano na MOI na amemhakikishia Prof. Yuanil kuwa Serikali ipo tayari kutoa ushirikiano zaidi utakaowezesha MOI kuongeza uwezo wake wa kutoa huduma za upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu kwa Watanzania ambao wamekuwa wakikosa huduma hiyo ama kulazimika kutumia gharama kubwa kwenda nje ya nchi kutibiwa.

Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na taarifa za kufanyika kwa mafanikio kwa upasuaji wa kwanza uliofanywa na Daktari Bingwa Prof. Yuanil hapo jana na kwamba anaamini wataalamu zaidi wataendelea kuja hapa nchini kutoka PUIH kwa ajili ya kutoa huduma na kuwafundisha madaktari wa Tanzania, na pia Watanzania wengi watakwenda nchini China kujifunza upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu.

Kwa upande wake Prof. Yuanil amempongeza Rais Magufuli kwa juhudi zake kubwa za kuhakikisha MOI inaimarishwa ikiwemo kufanya uwekezaji mkubwa katika miundombinu na amemhakikishia kuwa PUIH itahakikisha makubaliano yaliyotiwa saini mwaka jana kati ya hospitali hiyo na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto yanatekelezwa kikamilifu.